HABARI

HABARI

HABARI

HABARI

HABARI

HABARI

HABARI

DC. MUSSA KILAKALA AIOMBA TUME YA KUREKEBISHA SHERIA KUFUNGUA TAWI MOROGORO

 

Mkuu wa wilaya ya Morogoro Mh. Mussa R. Kilakala alipotembelea banda la Tume hiyo katika Maonesho ya kibiashara yaliyoratibiwa na Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) yanayofanyika katika Uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro Novemba 24, 2025 .

Mkuu wa wilaya ya Morogoro Mh. Mussa R. Kilakala, ameomba Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania, kuweka tawi la ofisi yao Manispaa ya Morogoro ili kusaidia wananchi elimu ya kisheria kuhusu changamoto mbalimbali za kisheria wanazopitia.

Mhe.Kilakala aliyasema hayo Novemba 24, 2025 alipotembelea banda la Tume hiyo katika Maonesho ya kibiashara yaliyoratibiwa na Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) yanayofanyika katika Uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro.

Akizungumza kueleza kuhusu changamoto za kisheria zinazowakabili wananchi wa Morogoro, Mkuu huyo wa Wilaya alisema kumekua na wimbi kubwa la migogoro ya wakulima na wafugaji ambao usuluhishi wake ni kupatiwa elimu ya kisheria ambapo alieleza wengi wao hawana ufahamu, jambo linalopelekea migogoro hiyo kujirudia rudia.

"Sisi hapa tuna Wafugaji na Wakulima wana migogoro ya kisheria kila siku nadhani Tume mlitakiwa muwe na tawi hapa kutusaidia kuwaelimisha" alisema Mh. Kilakala.

Afisa Sheria kutoka Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania, Bi. Jackline Nungu, alisema licha ya kutokua na tawi mkoani hapo bado wananchi wanayo nafasi ya kutumia kipindi hiki cha maonesho kufika bandani hapo kujifunza kuhusu sheria mbalimbali na kueleza kuwa Tume hushiriki katika kampeni na maonesho mbalimbali ili kutoa elimu ya sheria na msaada wa sheria kwa wananchi.

Aidha Jackline aliongezea kuwa kutokana na kukua kwa teknolojia ya habari na mawasiliano, Tume imekua ikitoa elimu kupitia  vyombo vya Habari kama vile, vituo vya redio, televisheni na Magazeti na kuwafikia wananchi wengi zaidi kwa pamoja.

Aidha alieleza kuwa wananchi pia wanaweza kuwafuatilia kupitia tovuti, na anuani za mitandao ya kijamii ili kuendelea kuchangia na kutoa maoni yao ya mapendekezo ya marekebisho ya sheria mbalimbali.

"Tunazo anuani zetu wananchi pia wanaweza kutufuatilia na kutoa maoni tovuti yetu ni www.lrct.go.tz , na kwa mitandao ya kijamii instagram na facebook ni tumesheria.tanzania"  alimaliza akieleza Jackline.

Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania inashiriki Maonesho ya Kibiashara Mkoani Morogoro kwa ajili ya kutoa elimu ya sheria kwa Umma ambapo Maonesho hayo yalianza Novemba 20, 2025 na kutegemewa kuhitimishwa Novemba 30, 2025.

KATIBU MKUU MASWI AHIMIZA UBUNIFU KAZINI, AFUNGUA MKUTANO WA BARAZA LA WAFANYAKAZI LRCT

 

Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Eliakimu Maswi  wakati wa hotuba yake aliyoitoa  kwa watumishi wa Tume ya Kurekebisha sheria Tanzania wakati wa Baraza la Wafanyakazi lililofanyika tarehe 19.11.2025 katika ukumbi wa mikutano katika hoteli ya Sanaan iliyopo Dodoma Mjini.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Eliakimu Maswi, amewataka watumishi wa Tume ya kurekebisha Sheria Tanzania   kuongeza ubunifu na kutumia maarifa mapya katika kutekeleza majukumu yao ili kuongeza ufanisi na kuendana na mabadiliko ya kiutendaji ndani ya Serikali.

Maswi alitoa wito huo tarehe 19/11/2025 wakati akifungua Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi uliofanyika katika Hoteli ya Sanaan, Jijini Dodoma, Kikao kilichowakutanisha wajumbe wa baraza la wafanyakazi watumishi mbalimbali kutoka ngazi mbalimbali za TUGHE Taifa na Mkoa.

Akizungumza wakati wa ufunguzi huo, Maswi alisema Tume   ina nafasi muhimu katika uimarishaji wa misingi ya utawala bora, hivyo watumishi wanapaswa kuongeza ubunifu katika utatuzi wa changamoto, utafiti , na utoaji wa huduma kwa wananchi.

“Watumishi lazima wabuni mbinu mpya za kufanya kazi, kutumia teknolojia ipasavyo, na kufikiri nje ya mipaka ya kawaida. Ubunifu ndiyo msingi wa kuongeza matokeo na kuboresha huduma kwa wananchi,” alisema Maswi.

Aliongeza kuwa ubunifu si jukumu la idara fulani tu, bali ni wajibu wa kila mtumishi, kuanzia ngazi ya chini hadi ya juu. Alisisitiza kuwa Serikali inategemea mawazo mapya kutoka kwa watumishi wake ili kuharakisha maboresho ya mifumo ya sheria na haki.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi  Bw. George Mandepo alieleza kwamba Tume  kwa mwaka wa fedha 2025/26 imejipanga kufanya utafiti juu ya mfumo wa sheria zinazohusiana na biashara ya jewa ukaa, utafiti  kuhusu mfumo wa sheria zinazoehusiana na teknolojia ya akili unde na mapitio ya sheria ya Bima za magari sura ya 169.

 Aidha, kazi nyingine ni mapitio ya sheria ya bima sura 394 na mapitio ya sheria iliyoanzisha Tume ya kurekebisha sheria Tanzania sura ya 171 alieza Mandepo

Hata hivyo  Bw. Mandepo alisema Tume kwa kushirikiana ofisi ya mwanashria mkuu wa Serikali na Wizara ya Katiba na sheria wameunda kikosi kazi ambacho kinaendelea na uchambuzi wa sheria za kipaumbele na uandaaji wa bajeti kwa ajili ya utekelezaji ili kuhakikisha Dira inafikia malengo tarajiwa.

 

KAMISHNA AWASHAURI WATAFITI WA TUME YA KUREKEBISHA SHERIA KUWAFIKIA WANANCHI WA KAWAIDA

 

Kamishna wa Tume ya Kurekebisha Sheria, Bw. Iddi Mandi wakati wa Baraza la wafanyakazi lililofanyika tarehe 18.11.2025 katika hoteli ya Sanaan Mjini Dodoma 

Kamishna wa Tume ya Kurekebisha Sheria, Bw. Iddi Mandi, ametoa wito kwa wataalamu na watafiti wa tume hiyo kuhakikisha kuwa wanapata maoni ya wananchi wa kawaida wakati wa tafiti wanazozifanya ili kuhakikisha maboresho ya sheria yanayopendekezwa yaweze kuwa na manufaa kwa jamii nzima.

Akizungumza wakati wa wasililisho lake kuhusu utafiti wa Kisheria kwa wajumbe wa Baraza la wafanyakazi la Tume hiyo lilofanyika leo tarehe 18. /11/2025 katika ukumbi wa mikutano wa Hoteli ya Saanan Jijini Dodoma, Bw. Mandi alisema kuwa tafiti nyingi za kisheria zinapoishia kufanywa kwenye Taasisi, Wizara mbalimbali na watu mashuhuri, hupunguza uhalisia wa changamoto zinazowakabili wananchi wengi wanaoishi katika maeneo ya pembezoni na miji.

“Ni muhimu tafiti zetu ziwe za kina na zenye uwakilishi mpana. Tunapaswa kuwafikia wananchi wa kawaida, maana wao ndio wahanga wakuu wa sheria tunazozifanyia marekebisho. Hatutaki sheria zinazobaki kwenye makaratasi bila kuwa na uhalisia kwenye maisha ya watu,” alisema Bw. Mandi.

Amesisitiza kuwa ufanisi wa tume hiyo unategemea uwezo wake wa kuwasikiliza wananchi, kuelewa mahitaji yao, na kuyatumia kama msingi wa mapendekezo ya mabadiliko ya sheria.

Kwa mujibu wa Kamishna Mandi, tafiti za kisheria zinapaswa kuwa chombo cha kuhakikisha haki inatendeka na kwamba sheria zinakidhi mahitaji ya kizazi cha sasa bila kupoteza misingi yake ya kulinda maslahi ya umma.

Bw. Mandi ameitaka timu ya utafiti ya tume hiyo kubuni mbinu shirikishi, ikiwemo kufanya mikutano ya hadhara, kutembelea vijiji na vitongoji, pamoja na kuendesha majadiliano na makundi mbalimbali ya jamii ili kupata maoni mapana kabla ya kuandaa mapendekezo rasmi ya marekebisho ya sheria.

Tume ya Kurekebisha Sheria inaendelea na mchakato wa mapitio ya sheria mbalimbali nchini, ambapo ushiriki wa wananchi umetajwa kuwa nguzo muhimu katika kufanikisha marekebisho yenye tija na yanayotekelezeka.

Kikao cha Baraza la wafanyakazi Tume ya Kurekebiha Sheria Tanzania kilihudhuriwa na wajumbe kutoka idara mbalimbali za tume  hiyo na wageni kutoka Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE) taifa na Mkoa.

Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania Yakutana na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Zanzibar Kujadili Utekelezaji wa Mkataba wa Ushirikiano (MoU)




Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania   na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Zanzibar wakati wa kikao kazi cha kuimarisha utekelezaji wa mkataba wa makubaliano ya ushirikiano (MoU) kati ya pande hizo mbilli uliofanyika katika ofisi hizo mjini Zanzibar

Katibu Mtendaji Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania ( kushoto) akisisitiza jambo wakati wa Kikao kazi kilichofanyika Zanzibar, pembeni ni Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Zanzibar Bw. Shaaban Abdalla.
Kikao kinaendelea 













Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania   imekutana na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Zanzibar katika kikao kazi kilicholenga kuimarisha utekelezaji wa mkataba wa makubaliano ya ushirikiano (MoU) kati ya pande hizo mbili, kwa lengo la kuimarisha ushirikiano  katika mapitio, maboresho, na utafiti wa sheria zinazotekelezwa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Kikao hicho kilichofanyika  Zanzibar na kuhudhuriwa na wajumbe kutoka Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania pamoja na maafisa waandamizi kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Zanzibar kilijadili  mafanikio yaliyopatikana tangu kutiwa saini kwa makubaliano hayo, pamoja na kuweka mikakati ya pamoja ya utekelezaji wa maeneo ya kipaumbele ya kisheria kwa kipindi kijacho.

Akizungumza katika kikao hicho, Katibu Mtendaji wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzani George Mandepo, alisema kuwa ushirikiano kati ya Tume na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Zanzibar ni muhimu katika kuimarisha mfumo wa sheria nchini kwa kuzingatia mahitaji ya pande zote mbili za Muungano.

Kupitia mkataba huu wa makubaliano, tunajenga msingi madhubuti wa kushirikiana katika kufanya tafiti za kisheria, kubadilishana uzoefu, na kuimarisha uwezo wa wataalamu wetu wa sheria kutoka pande zote mbili,alisema.

Aidha Bw. Mandepo alisema kwamba LRCT kwa mwaka wa fedha 2025/26 imejipanga kufanya tafiti mbalimbali ikiwemo utafiti wa mfumo wa sheria zinazosimamia upingaji wa maamuzi ya kiutawala mahakamani,utafiti wa mfumo wa sheria zinazosimamia usajili wa Mawakili Tanzania na utafiti wa mfumo wa sheria unaosimamia biashara ya hewa ukaa.

Bw. Mandepo amefafanua kwamba Tume  kwa sasa inaendelea kufanya mapitio ya sheria ya Bima sura ya 169, mapitio ya sheria ya Bima sura ya 394 na mapitio katika sheria ya afya na usalama mahala pa kazi Sura ya 297.

Hata hivyo alieleza kwamba Tume inafanya tathmini ya utekelezaji wa sheria za mamlaka ya nchi kuhusu umilikimali na maliasili za nchi sura ya 449 pamoja na sheria ya mapitio na majadiliano  kuhusu masharti hasi katika mkataba wa mali asili na maliasilia  sura ya 450.

Eneo lingine ambalo limetajwa kufanyiwa tahmini ni katika utekelezaji wa sheria ya ugaidi sura ya 19 sambamba na utoaji wa elimu ya sheria kwa Umma na uandaaji wa machapisho pamoja na ushiriki wa maonesho mbalimbali hapa nchini alimalizia Katibu Mtendaji.

Kwa upande wake, Naibu Mwanasheria Mkuu Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Zanzibar, Bw. Shaaban Abdalla, alieleza kuwa ushirikiano huo unaongeza tija katika kazi za uhuishaji wa sheria kwa kuhakikisha kwamba mabadiliko ya kisheria yanayoletwa yanazingatia uhalisia wa jamii zote.

Tunaamini kuwa kazi za mapitio ya sheria zinahitaji ushirikiano wa karibu kati ya taasisi zote za kisheria katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ushirikiano huu utasaidia pia kuondoa migongano ya kisheria na kujenga msingi wa sheria zinazotekelezeka kwa haki na usawa,alisema.

Katika kikao hicho, wajumbe walikubaliana pia kuunda kikosi kazi cha pamoja kitakachoratibu utekelezaji wa maeneo ya kipaumbele yaliyobainishwa katika MoU, ikiwemo masuala ya sheria za teknolojia, haki za binadamu, usuluhishi wa migogoro, na sheria za kimataifa zinazogusa pande zote za Muungano.

MoU kati ya Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Zanzibar ilisainiwa kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa kitaalamu, kubadilishana taarifa, na kujengeana uwezo katika nyanja mbalimbali za kisheria, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhakikisha maendeleo ya sheria yanaenda sambamba na mabadiliko ya kijamii, kiuchumi na kiteknolojia.

MWISHO

 

TUME YA KUREKEBISHA SHERIA YAPANGA MIKAKATI YA KUTEKELEZA DIRA YA TAIFA 2050





Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania (LRCT) leo tarehe 7 Agosti, 2025 imeeleza namna ilivyojipanga kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050 kwa kufanya maboresho katika mifumo ya sheria ili kuhakikisha inakidhi mahitaji ya vizazi vijavyo na kuendana na mabadiliko ya teknolojia, jamii na mazingira duniani.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, Naibu Katibu wa Tume hiyo, Bi. Zainab Chanzi, alisema kuwa Dira ya Taifa ya 2050 ni dira pana na ya kipekee inayolenga kuiwezesha Tanzania kuwa Taifa jumuishi lenye ustawi, haki na linalojitegemea.

“Ili Dira ya 2050 iweze kufikiwa, sheria ni nyenzo muhimu katika utekelezaji wa Dira, hivyo sheria zetu lazima ziakisi misingi, nguzo na shabaha za Dira hiyo. Kama Tume, tumejipanga kuhakikisha sheria zinafanyiwa mapitio, tafiti na tathmini na wananchi kuelimishwa maboresho ya sheria kwa lengo la kujenga uelewa kwa wananchi,” alisema Bi. Chanzi.

Aidha Bi. Chanzi alibainisha mikakati mbalimbali ambayo Tume imepanga kutekeleza imiwemo kupitia Sheria zilizopitwa na wakati ili kuhakikisha hazikwamishi maendeleo ya kisasa kama vile matumizi ya akili unde (AI).

Akizungumzia kuhusu sekta ya Kilimo Bi. Zainab alieleza umuhimu wa Sekta ya Kilimo kwa kuwa kwa mujibu wa Dira 2050 ni miongoni wa sekta ya mageuzi hivyo kama Tume imejipanga kuhakikisha sheria zinazosimamia sekta hii zinaakisi matarajio yaliyowekwa na Dira kama vile kuwa Taifa linaloongoza katika uzalishaji wa chakula.


“Sheria tunazotunga leo ndizo zitakazojenga Tanzania ya baadaye. Hivyo basi, kazi yetu ni kuhakikisha msingi huo wa kisheria unawekwa kwa weledi, umakini na mshikamano wa kitaifa,” aliongeza.

Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania Yatoa Elimu ya Sheria ya Ustawi wa W...

KARIBUNI NANENANE TUWAHUDUMIE