HABARI

HABARI

HABARI

HABARI

HABARI

HABARI

HABARI

TUME YA KUREKEBISHA SHERIA TANZANIA YAKABIDHI TAARIFA MBILI (2) ZA UTAFITI NA MAPITIO YA SHERIA KWA WAZIRI DKT. DAMAS NDUMBARO.







Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania imekabidhi Taarifa mbili (2) za Utafiti na Mapitio ya Sheria zilizofanyika katika mwaka wa Fedha 2023/2024 na 2024/2025. Kwa Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Damas Ndumbaro ili kuruhusu hatua zingine kuendelea juu ya sheria hizo.

Taarifa hizo ni Taarifa ya Mapitio ya Sheria ya Takwimu, Sura ya 351; na Taarifa ya Utafiti kuhusu Mfumo wa Sheria zinazosimamia Vyama vya Ushirika, ambazo zimekabidhiwa tarehe 24 Machi 2025 katika ukumbi wa mikutano wa Wizara ya Katiba na sheria Mji wa Serikali Mtumba Jijini Dodoma.

Akizungumza mara baada ya kupokea Ripoti hizo Waziri wa Katiba na Sheria Dkt Damas Ndumbaro licha ya kupongeza juhudi kubwa zinazofanywa na Tume ya kurekebisha Sheria Tanzania, alisema Tume hiyo ndiyo Taasisi kuu ya Utafiti wa Sheria nchini na ndiyo yenye mamlaka kisheria kufanya mapitio na kupendekeza maboresho ya sheria yenye tija na ya kudumu ili sheria hizo ziendane na wakati.

Katika hatua hiyo Dkt. Ndumbaro alieleza wazi kuhusu utekelezaji wa 4R za Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kwamba Tume inatekeleza kwa vitendo kwa kufanya tafiti na Mapitio ya kisheria akibainisha kufanya hivyo ni kutimiza jukumu hilo kwa usahihi kwa kufanya tafiti, mapitio na  tathmini  zinazolenga maendeleo ya nchi kulingana na mabdiliko ya kijamii na kiuchumi duniani.

“Ninaamini kuwa mapendekezo yaliyotolewa katika taarifa hizi yatakidhi  kiu na matarajio ya wananchi na wadau mbalimbali ili kuleta mabadiliko ya namna ya utendaji na utoaji huduma kwa wananchi wa  taasisi zetu nchini.”

Awali alipozungumzia kuhusu maandalizi ya taarifa hizo Mwenyekiti wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzani Jaji wa Mahakama ya Rufani Mhe, Winifrida Korosso alisema Mchakato wa uandaji wa taarifa hizo umehusisha hatua mbalimbali za kitafiti ikiwemo vikao vya majadiliano na wadau (Stakeholders Consultative Meetings), uchambuzi wa hoja za awali, mapitio ya makala , machapisho, nyaraka, sera, sheria za ndani na sheria za nchi nyingine. Aidha Tume imepitia  mikataba ya kimataifa na kikanda, na kueleza kuwa Wadau mbalimbali wameshiriki katika kila kazi ya Utafiti na Mapitio.

Akieleza zaidi kuhusu taarifa ya Mapitio ya Sheria ya Takwimu , Mhe. Korosso alisema Tume imebaini kuwapo kwa changamoto za kisera, kisheria na kiutawala zinazochangia kukosekana kwa mazingira wezeshi ya uwasilishaji wa takwimu rasmi NBS ambayo  ndiyo taasisi inayoratibu Takwimu nchini na Msimamizi wa Kanzidata ya Taifa ya Takwimu rasmi nchini.

 Kwa upande wa Taarifa Utafiti kuhusu Sheria zinazosimamia Vyama vya Ushirika zikibainika changamoto kadhaa zikiwamo Kukosekana kwa mfumo madhubuti wa kusimamia mitaji, fedha, mali na madeni ya vyama vya ushirika nchini.

“Aidha pamoja na changamoto hizo na zinginezo zilizoanishwa katika taarifa Tume imetoa mapendekezo ya namna ya kukabiliana na changamoto hizo” alisema Mhe. Korosso kwa msisitizo.

Kwa upande wake Bw. Gerge Mandepo ambaye ni Katibu Mtendaji wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania alisema mpaka sasa Tume hiyo imeshawasilisha jumla ya Taarifa 11 za sheria mbali mbali katika kipindi cha 2023/2025 na kuahidi kuongeza bidii ya kuzipitia sheria nyingi zaidi ili kuleta mabadiliko yenye tija.

“ ..tunashukuru kwa Wizara ya Katiba na Sheria kutuongezea bajeti ya 46% sasa, hii inatupa nguvu kuongeza kasi ya kuzifanyia marekebisho sheria nyingi zaidi kwa kufanya tafiti, mapitio na tathmini ili kuongeza tija katika sheria mbali mbali” alisema Mandepo.

Waziri wa Katiba na Sheria azitaka Wizara na Taasisi Nchini Kufanya kazi na Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania.

 



Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt  Damas Ndumbaro, amezitaka Wizara na Taasisi zinazohitaji Kurekebisha au kutunga  sheria  kuitumia Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania  kufanya utafiti kwa kuwa ndio Taasisi ya Serikali yenye dhamana ya kisheria ya kufanya tafiti za marekebisho au maboresho ya Sheria. 


Kauli hiyo ameitoa leo tarehe 24.03.2025 katika ukumbi wa Bunge wakati akiwasilisha taarifa ya Wizara hiyo kwenye Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria. Amesema  kwamba zipo taasisi ambazo zimekuwa zikileta mapendekezo ya kutunga au kurekebisha sheria Bungeni bila kuzingatia takwa kufanya utafiti wa kina jambo ambalo huchangia sheria hizo kupoteza uhalisia ndani ya kipindi kifupi.


“zipo wizara ambazo zimekuwa zileta sheria mbele ya kamati posipokufanyiwa utafiti wa kisheria, ndani ya Serikali, Mtafiti wa Sheria anayetambulika kwa mujibu wa Sheria za Nchi  ni Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania " Alisema Mhe. Ndumbaro.



Amesema kuwa, Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania ndio chombo maalumu kinachotambulika ki sheria  kwa kufanya  utafiti kuhusu sheria zote hapa nchini na sio vyuo vikuu kama wanavyofanya na baadhi ya Wizara na Taasisi mbalimbali na hatua hizo zimekuwa zikifanyika pengine kwa kutumia gharama kubwa na hatimaye Sheria zinazokusudiwa kukosa tija zinapotungwa 


Alisisitiza kwamba, ili kufanikisha mabadiliko bora ya Sheria, Wizara na Taasisi za Serikali  zinazohitaji kuboresha au kubadilisha sheria, zinapaswa kuchukua hatua za kutumia Tume ya Kurekebisha Sheria kufanya tafiti na mapitio ya Sheria badala ya kuamua zenyewe bila kuwa na msingi wa kisheria kama ilivyo kwa Tume ya Kurekebisha Sheria ambayo inatekeleza majukumu hayo chini ya Sheria yake.


Alikumbusha kwamba, kwa kutumia Tume, mchakato wa mapitio na mabadiliko ya sheria unaweza kufanyika kwa haraka na kwa ufanisi mkubwa, alisistiza Mhe Dkt. Ndumbaro .

Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania yashiriki kikamilifu maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani

 








Wanawake watumishi kutoka Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania wameshiriki maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani ambapo kimkoa yamefanyika katika viwanja vya Chinangari Park Jijini Dodoma.  

 Akizungumza mara baada ya maadhimisho hayo leo Machi 8,2025 Afisa Ugavi wa Tume hiyo Bi. Aneth Lyatuu amesema kuwa siku ya leo inawakumbusha na kuwapa ujasiri zaidi wa kuweza kusimamia malengo ambayo wamejiwekea katika akili zao. 

  "Siku ya leo niwaambie wanawake wenzangu tujitahidi kupendana ,mwenzako akikukasirisha mwambie, msamehe na tusonge mbele pia tutiane moyo na nguvu,"amesema.  

 Aidha amesema kupitia maadhimisho hayo wanawake wasisahau maadili ya watoto kwasababu wanawake ndiyo wanaoongoza jamii na inaanzia katika familia na wakisimama imara jamii yote itaimarika. 

  Maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani kitaifa yamefanyika Jijini Arusha ambapo yameongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Mtazamo wa Jaji Winifrida Korosso kufuatia Maadhimisho ya wiki ya Sheria

JAJI WINIFRADA KOROSSO ATEMBELEA UWANJA WA MAADHIMISHO YA SIKU YA SHERIA...

PROF. ELISANTE OLE GABRIEL ATEMBELEA BANDA LA TUME YA KUREKEBISHA SHERI...

Mabaraza ya wafanyakazi yatumike Kujenga Demokrasia sehemu za kazi - Kabudi



Mabaraza ya  wafanyakazi yanapaswa kutumika kama chombo muhimu katika kuboresha na kuimarisha demokrasia kwenye eneo la kazi badala ya kutumika pekee kukusanya na  kupitia maoni ya watumishi .


Kauli hiyo imetolewa tarehe 14/11/2024 na Waziri wa Katiba na Sheria Prof. Palamagamba Kabudi katika ukumbi wa mikutano wa Hoteli ya Midland iliyopo mjini Dodoma wakati akifungua kikao cha 21 cha baraza la wafanyakazi la Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania ambapo ameleleza mabaraza hayo  yanahusisha ushirikishwaji wa wafanyakazi katika maamuzi ya Taasisi au shirika wanamofanyia kazi jambo ambalo  huongeza uwazi na uwajibikaji.

Waziri Kabudi ameipongeza Manejimenti ya Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania kwa kutimiza takwa la kisheria la kufanya kikao cha baraza huku akifafanua kwamba Baraza la Wafanyakazi halipaswi kuwa chombo cha kupokea malalamiko ya watumishi pekee ingawa ni muhimu kwa baraza hilo kushughulikia malalamiko na changamoto zinazowakabili wafanyakazi na badala yake  jukumu lake linapaswa kuwa pana zaidi. 

Prof amefafanua kwamba Baraza linaweza na linapaswa kuwa jukwaa la kuchochea maendeleo, kutoa maoni, na kutoa mawazo ya kuboresha ufanisi wa Taasisi kwa ujumla.

Demokrasia  katika eneo la kazi ni muhimu kwani inachochea ari ya kazi, kuimarisha ufanisi, na kujenga mazingira yenye amani na haki, alisistiza Waziri wa Kabudi.

“ Baraza la Wafanyakazi si tu chombo cha kusimamia haki za wafanyakazi, bali pia ni nyenzo muhimu ya kufanikisha malengo ya taasisi kupitia ushirikiano wa kweli na mawasiliano ya wazi” alisema Waziri 

Amesema  Baraza linatoa nafasi kwa wafanyakazi kutoa maoni, mawazo, na mapendekezo kuhusu masuala yanayohusu ustawi wao na maendeleo ya Taasisi kwa ujumla  hivyo kupitia Baraza la Wafanyakazi, viongozi watakiwa  kupata mawazo mapya ya kuboresha mazingira ya kazi.

Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Tume hiyo Bw. George Mandepo, alieleza kwamba kikao hicho ni hitaji la kisheria na ni muhimu kwa kuwa linashirikisha  wafanyakazi katika michakato ya kufanya maamuzi ili kuimarisha ufanisi wa kazi.


Aidha amefafanua kwamba Tume inatekeleza mipango mbalimbali ya kuhakikisha kwamba watumishi wanapata mafunzo  ili kuwajengea uwezo na kuboresha ufanisi  katika kutekeleza majukumu yao.

Mkutano huo uliwaleta pamoja wafanyakazi wa Tume na wadau wengine muhimu kwa lengo la kujadili masuala ya kazi, kubadilishana mawazo, na kutafuta suluhisho la changamoto zinazokabili sekta ya sheria.


MWISHO