Watumishi Watakiwa Kuimarisha Mawasiliano na Kuleta Mrejesho
Waziri wa Katiba na Sheria Balozi Dkt. Pindi Hazala Chana amezitaka taasisi zote ambazo zipo chini ya Wizara ya Katiba na Sheria kuimarisha
mawasiliano ya ndani na nje pamoja na kuleta mrejesho wa maagizo mbalimbali
yanayotolewa na Serikali.
Kauli hiyo ameitoa leo tarehe 15/04/2024 wakati wa ufunguzi
wa Kikao cha Baraza la Wafanyakazi la Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania
(LRCT) lililofanyika katika Ukumbi wa Mikutano uliyopo katika Chuo cha Uongozi
cha Mwalimu Nyerere kilichopo Kibaha, Mkoani Pwani.
Waziri Dkt. Pindi Chana amesema mawasiliano ni muhimu katika
kuendesha Serikali na kuelezea mafanikio ya Serikali kwa wananchi hivyo ni
muhimu mawasiliano yakaimarishwa na kusaidia kufikisha ujumbe uliokusudiwa kwa
wakati.
Aidha ameagiza watumishi wote waliopo chini ya Wizara hiyo
kuhakikisha wanatoa mrejesho wa utekelezaji wa maagizo ya Serikali huku
akibainisha kwamba kila jukumu au agizo liwekewe ukomo wa muda utekelezaji
(deadline) ili kuongeza tija katika usimamizi wa majukumu.
“Viongozi wanapotoa maagizo kwa watumishi, watumishi hao
wanapaswa kuyatekeleza kwa wakati na sio kusubiri mpaka wakumbushwe kuhusu
utekelezaji huo. Vile vile wanatakiwa baada ya kutekeleza maagizo hayo kutoa
mrejesho wa utekelezaji huo ili kukamilisha msingi mzima wa mawasiliano” Dkt.
Pindi Chana.
Hata hivyo Waziri amewaomba watumishi wote kuhakikisha
wanatumia haki yao ya Kikatiba kwa kushiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa kuchagua
viongozi ili kutimiza haki yao ya kikatiba na hivyo kukuza kidemokrasia.
Awali akimkaribisha
Waziri huyo, Katibu Mtendaji Tume wa Kurekebisha Sheria Tanzania Bw. George
Mandepo ameeleza kuwa katika Mkutano huo mada mbalimbali yatajadiliwa yakiwemo
Maboresho ya Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini ya mwaka 2004; Mabadiliko ya
Kanuni za Utumishi wa Umma za mwaka 2022; Maboresho ya Mifumo ya TEHAMA na
Umuhimu wake katika Uendeshaji wa Shughuli za Serikali; na Mwenendo wa
Maboresho ya Muundo wa Tume ya Kurekebisha Sheria.
Aidha, Katibu
Mtendaji Bw. Mandepo ameeleza kwamba Tume imeweza kutekeleza majukumu
mbalimbali kama yalivyopangwa katika Mpango na Bajeti wa mwaka 2023/2024 ikiwa
ni pamoja na kukamilisha Taarifa ya Utafiti wa Mfumo wa Sheria Unaosimamia Makosa
Dhidi ya Maadili. Tume inaendelea kutekeleza Mpango na Bajeti wa mwaka
2023/2024 kwa kukamilisha Taarifa za Mapitio ya Mfumo wa Sheria Unaosimamia
Dhamana, Taarifa ya Mapitio ya Adhabu ya Viboko, Taarifa ya Tathmini ya
Utekelezaji wa Sheria za Sekta ya Usafiri Ardhini, Taarifa ya Tathmini ya
Utekelezaji wa Sheria Zinazosimamia Hakimilki na Hakishiriki, na Taarifa ya
Utafiti wa Mfumo wa Sheria Unaosimamia Makosa ya Uhujumu Uchumi na Uhalifu wa
Kupangwa alieleza Katibu mtendaji huyo.
MWISHO






No comments: