Wakili wa Serikali katika Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania Ismail Hatibu akipokea maelekezo kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Njombe Antony Mtaka jana wakati alipotembelea banda la Tume hiyo kwenye maonesho ya Nanenane mkoani Mbeya.
Wakili wa Serikali katika Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania Ismail Hatibu akitoa maelezo kwa wananchi walitembelea banda la tume hiyo.
Mkuu wa Mkoa wa Njombe Mh. Anthony Mtaka, leo ameipongeza Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania (LRCT) kwa namna wanavyoisaidia jamii katika suala zima la mabadiliko ya sheria kwa kushirikisha jamii za watanzania kutoa maoni na mapendekezo ya mabadiliko ya Sheria mbalimbali ili kuakisi na kukidhi maslahi yao.
Pongezi hizo amezitoa leo wakati wa maadhimisho ya sikukuu ya wakulima Nanenane yanayofanyika kitaifa Katika uwanja wa Nanenane uyole Mkoani Mbeya alipotembelea Banda la Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania ambapo ameeleza kufurahishwa na kazi wanayoifanya ya kupokea maoni ya wananchi na kuyafanyia kazi ki sheria.
Aidha Mtaka ameshauri Tume hiyo kuwa karibu na wananchi ili waweze kutoa maoni mbalimbali kwa kuwa maendeleo ya nchi hutegemea msingi wa sheria zilizo bora na na namna zinavyoweza kuwasaidia wananchi.
Amesema Tume inapaswa kuongeza wigo wa kujitangaza kupitia vyombo vya habari mitandao ya kijamii pamoja na kukutana na wananchi mara kwa mara kila ili kutoa elimu ya Sheria mbalimbali ambazo zimebadilishwa. Aidha, amesisitiza pia elimu hiyo izidi kutolewa katika maeneo mengi nchini ili wananchi wanaoishi mijini na vijijini wajue haki na wajibu wao kisheria.
Akitolea mfano Sheria ya Ndoa, RC Mtama amesema wapo baadhi ya vijana wamekuwa wakikosa fursa za kuendelea na masomo kwasababu ya kuolewa wakiwa na umri mdogo suala ambalo linakosesha maendeleo ya vijana na taifa kwa ujumla.
Vile vile, ameiomba Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania kuangalia sheria na taratibu kwa watumishi wa umma endapo sheria kama inaweza kuwaondoa katika utumishi pindi wanapobainika kufanya vitendo vya ushoga au usagaji na makosa mengine dhidi ya maadili nchini Tanzania.
"Ningependa Sheria iweke wazi endapo itabainika kwamba Kuna mtumishi wa umma anafanya vitendo vya ushoga au usagaji na makosa mengine dhidi ya maadili waweze kufukuzwa kazini kwasababu Sheria haisemi chochote kwa watumishi wa namna hiyo" Mtaka.
Kwa upande wake wakili wa Serikali Bw. Ismail Hatibu amesema tayari Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania ipo katika hatua za mwisho za uchakataji wa maoni ya wadau katika uandaaji wa taarifa ya Mfumo wa Sheria dhidi ya Maadili Tanzania ambapo itagusa maeneo yote yanayolalamikiwa.
Wakati huo huo, Bw. Hatibu amemueleza RC Mtaka kwamba kwa sasa Tume inatoa elimu ya sheria kwa umma kupitia radio, luninga, magazeti na mitandao ya kijamii. Aidha, ameeleza pia Tume hutoa elimu hiyo ya sheria kwa kufanya makongamano, warsha na semina kuhusu sheria mbalimbali.
Wakili Hatibu alieleza pia kwa sasa taarifa Tume zinaandaliwa kwa lugha ya kiswahili ili watanzania wengi waweze kuzielewa taarifa hizo.
No comments: