TUME ya Kurekebisha Sheria Tanzania imewasilisha taarifa mbili za mapitio ya
mfumo wa sheria unaosimamia makosa dhidi ya maadili na taarifa ya mapitio ya mfumo
wa sheria unaosimamia udhamini hapa
nchini baada ya kufanyiwa utafiti wa kina.
Ripoti hizo zimekabidhiwa jana tarehe 22.09.2023 kwa Waziri
wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Pindi Chana baada ya kufanya ziara katika ofisi
ya Tume hiyo na kukutana na watumishi
kwenye ukumbi wa mikutano uliopo katika majengo ya chuo kikuu cha Dodoma (udom)
ambapo alipitishwa na kupokea taarifa hizo.
Akiongea kabla ya kukabidhi taarifa hiyo kwa waziri
Mwenyekiti wa Tume hiyo Jaji Mstaafu
January Msofe amesema katika kukamilisha mapitio ya Sheria zinazohusu makosa
dhidi ya Maadili Tume ilikusanya maoni ya wadau mbalimbali katika mikoa 18 ikiwemo Dodoma, Singida, Mwanza, Mara, Dar es
Salaam, Katavi, Geita, Shinyanga, Pwani, Tanga, Iringa, Mbeya, Arusha, Manyara,
Mtwara, Lindi, Tabora, Ruvuma na Kigoma.
Jaji Msofe amesema
waliohojiwa ni pamoja na majaji, mahakimu, waendesha mashtaka, mawakili
wa kujitegemea, wapelelezi, maafisa ustawi wa jamii, viongozi wa dini, walimu
wa shule za sekondari na msingi, watendaji wa mitaa, na asasi za kiraia
zinazotoa msaada wa kisheria.
Aidha Jaji huyo ameeleza kwamba utafiti kuhusu makosa dhidi
ya maadili ulibainisha kwamba makosa
haya yanaongezeka siku hadi siku jambao ambalo limekuwa tishio kwa taifa .
“ katika mwaka wa 2021 jumla ya makosa 7,601 ya kubaka na
kulawiti yaliripotiwa na mwaka 2022 makosa 8,413 yaliripotiwa. Hata hivyo, kesi
zinazofunguliwa mahakamani ni chache kuliko zile zinazotolewa taarifa katika
vituo vya polisi, kwa mfano katika
kipindi cha 2021/2022 na 2022/2023 Ofisi ya Taifa ya Mashtaka ilifungua
Mahakamani kesi 2980 na 4,294 za makosa
dhidi ya maadili yakiwemo ya ukatili, kubaka, kujaribu kubaka, kulawiti na
kujaribu kulawiti” alisema Mhe. Jaji Msofe.
Mwenyekiti amemueleza waziri wa katiba kwamba kwa mujibu wa
utafiti kuna idadi kubwa ya kesi za makosa ya dhidi maadili ambayo hayajaripotiwa katika vyombo husika
huku akibainisha kwamba , makosa dhidi ya maadili yanayotokea mara kwa mara
katika jamii ni ubakaji; ulawiti; utoroshaji wa wasichana na walio na umri wa
chini ya miaka 16 na shambulio la aibu.
Akizungumzia taarifa ya mfumo wa
sheria unaosimamia udhamini amesema
utafiti umebaini kwamba baadhi ya watuhumiwa wa makosa dhidi ya maadili
wanaopewa dhamana huruka dhamana hususan watuhumiwa waliopo katika mikoa ya
mipakani, hushiriki katika kuharibu ushahidi kwa kuwatisha mashahidi na kurudia
makosa ya aina ile ile waliyoshtakiwa nayo.
Akimalizia hotuba yake jaji Msofe
amesema kwamba utafiti huo umebainisha changamoto mbalimbali zikiwemo malalamiko kuhusu watoto kuchanganywa na watu
wazima gerezani na hivyo kujifunza mbinu mbalimbali za uhalifu na kuhatarisha maisha
yao; mahakama za watoto kukosa miundombinu rafiki kwa ajili ya kusikiliza kesi
za watoto; na uhaba wa maafisa ustawi wa jamii unaosababisha mashauri kuchelewa
kuisha mahakamani kutokana na takwa la kisheria la uwepo wa afisa huyo wakati
wa kusikiliza kesi za watoto.
Naye Waziri wa Wizara ya Katiba na
Sheria Dkt. Pindi Chana amepongeza Tume
ya Kurekebisha Sheria Tanzania kwa jitihada wanazozifanya za kupitia sheria na
kuja na mapendekezo ambayo utekelezaji wake huheshimisha nchi ndani na nje .
Amesema utafiti uliofanyika kuhusu sheria
zinazosimamia maadili zitakuwa chachu
kwenye kuimarisha utamaduni mila na desturi pamoja na Kukuza uhusiano baina ya
mataifa ambapo ameeleza kwamba zitaimarisha amani na usalama katika taifa.
Hata hivyo amezipongeza taasisi za
kidini ambazo zimekuwa zikisaidia
kuimarisha maadili ya watanzania na kuahidi kuendelea kushirikiana na
vyombo vya dini katika kuimarisha amani.
“naipongeza sana Tume ya Kurekeibisha
Sheria kwa namna wanavyojitahidi kutafiti sheria na kuja na mapendekezo muhimu,
mapendekezo mnayotuletea yamekuwa chanzo cha utulivu wa taifa na zimesisimua
ukuaji wa uchumi hapa nchini” Dkt. Pindi Chana.
Hata hivyo Dkt. Pindi Chana ametoa
wito kwa watanzania wote kutofumbia macho pindi waonapo vitendo vya ukiukwaji
wa maadili au uvunjifu wa amani huku
akieleza kwamba Wizara ya Katiba na Sheria
imeendeLea kutoa msaada wa sheria kwa
wananchi kupitia kampeni ya Mama Samia legal aid Camping yenye lengo la
kuwafanya wananchi kufahamu sheria zinazowazunguka.
Awali akimkaribisha Mwenyekiti wa Tume
hiyo Jaji Griffin Mwakapeje amesema Tume hiyo imefanikiwa kuandaa ripoti
56 kuhusiana na sheria mbalimbali za hapa nchini huku akibainisha kwamba
taasisi hiyo imekuwa ikishirikiana na Taasisi mbalimbali za ndani na nje ya
nchi ili kufanikisha majukumu yake kwa ufanisi.
mwisho






No comments: