HABARI

HABARI

HABARI

HABARI

HABARI

HABARI

HABARI

» » TUMESHERIA YAINGIA DARASANI KUTOA ELIMU YA SHERIA











 TUME ya Kurekebisha Sheria Tanzania (LRCT) imeanza kutoa elimu kuhusu sheria mbalimbali  katika shule za msingi na sekondari za Mkoa wa Rukwa kwa  lengo la kuongeza uelewa wa sheria na utii wa sheria bila shuruti.


 Mkuu wa Kitengo  cha Elimu ya Sheria kwa Umma ambaye pia ni Naibu Katibu Mtendaji, Zainabu Chanzi, alisema miongoni mwa majukumu ya Tume hiyo ni kutoa elimu kwa umma ili kuisaidia jamii kuzielewa sheria na hivyo kupunguza utendekaji wa makosa mbalimbali  ya jinai.


Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana, Chanzi alisema elimu hiyo itakayotolewa kwa siku mbili katika shule za Manispaa ya Sumbawanga ni kuhusu Sheria ya Mtoto,Makosa dhidi ya Maadili ya Utu,Makosa ya Kimtandao, Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya.


Naye Katibu Tawala Mkoa wa Rukwa, Gerald Kusaya ameipongeza  Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania (LRCT) kwa uamuzi wake wa kutoa elimu hiyo kwa wanafunzi.


Kusaya alisema zoezi hilo litakuwa na  tija kubwa kwani jamii ina uhitaji mkubwa wa elimu ya sheria na kwamba  elimu hiyo itawasaidia watoto kufahamu haki na wajibu wao na kujiepusha kutenda makosa mbalimbali yaliyoanishwa katika sheria husika.


" Niwapongeze kwa uamuzi wa kutembelea wanafunzi na kuwapa elimu ili watambue haki na wajibu wao katika jamii, kwa kweli huduma yenu inahitajika sana Mkoani hapa" alisema.


Aidha, Katibu Tawala huyo ameiomba Tume hiyo kuendelea kutoa elimu hiyo kwenye shule na vikundi mbalimbali vya vijana na wajasiriamali kwa kuwa uelewa wa sheria utasaidia wananchi kutii sheria bila shuruti.


Kusaya alishauri elimu hiyo kuendelea kutolewa katika makundi mbalimbali ya jamii  bila kusuburi watende makosa na kufikishwa mahakamani.


«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post

No comments:

Tuandikie Maoni yako