Katibu
Mtendaji Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania (LRCT) Bw. George Mandepo ameiomba
Tume ya Kurekebisha Sheria ya Zanzibar kuendeleza ushirikiano wa Tume hizo hasa
katika kujengeana uwezo katika maeneo mbalimbali ya utekelezaji wa majukumu yao
ili kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa majukumu ya Tume hizo.
Rai hiyo
ameitoa leo tarehe 05/02/2024 wakati wa kikao kifupi kilichofanyika ofsini
kwake mara baada ya kutembelewa na Timu kutoka Tume ya Kurekebisha Sheria Zanzibar
ikiongozwa na Mkurugenzi wa Mapitio na Marekebisho ya Sheria Dkt. Mahfoudha
Masoud Ally ambapo waliweza kubadilishana nyaraka mbalimbali zikiwemo taarifa za
utafiti na majarida.
Bw. Mandepo
ameeleza kwamba “tuendelee kushirikiana hasa katika eneo la kujengeana uwezo
ili tuweze kufanya kwa ufanisi mkubwa kile ambacho kinatarajiwa ikiwa ni pamoja
na kubuni mbinu za kuwa “Proactive” badala ya “reactive” alisema Mandepo.
Kwa upande
wake Mkurugenzi wa Mapitio na Marekebisho ya Sheria wa Tume ya Kurekebisha
Sheria Zanzibar, Dkt. Mahfoudha Masoud Ally baada ya kubadilishana nyaraka
alisema, Tume ya Kurekebisha Sheria Zanzibar inatambua umuhimu wa ushirikiano
na Tume ya Kurekebisha Sheria hivyo basi nyaraka na machapisho waliyoyapokea yatakuwa
nyenzo muhimu katika utekelezaji wa majukumu ya Tume na hivyo kusaidia kupata
matokeo mazuri katika mchakato wa marekebisho ya sheria.
MWISHO






No comments: