Naibu Katibu Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania (LRCT) na Mkuu wa kitengo Cha Elimu ya Sheria kwa Umma Zainab Chanzi ametoa pongezi kwa Shule ya Sekondari Mazwi ya mkoa wa Rukwa kwa kushiriki uandishi wa aina mbalimbali za insha zenye lengo la kuelimisha jamii kuhusu athari za madawa ya kulevya, kupinga ukatili wa kingono na madhara ya matumizi hasi ya mtandao.
Pongezi hizo amezitoa leo ofisini kwake baada ya kupokea nakala tisa (9) za insha zilizopita mchujo wa kwanza kutoka kwa Mkuu wa shule hiyo Bw. Godson Mwaibingila ambapo Naibu Katibu alieleza kwamba baada ya kuzipokea wamezichuja na kupata washindi watatu kati ya tisa.
Wanafunzi waliofanya vizuri ni Lucy Mohamed Ally insha inayohusu athari za madawa ya kulevya Katika jamii, Shabani Alfred Mrisho aliyeshinda insha ya ukatili wa kingono na Neema Sigfrid Kapaya ambapo kila mmoja alipata zawadi ya Tsh. 30,000/
Zainab ameeleza kwamba uandishi wa insha hiyo ni matokeo ya elimu ya sheria waliyoitoa hivi karibuni walipotembelea mkoa wa Rukwa ambapo Tume ilitoa elimu ya Makosa dhidi ya Maadili,Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa ya Kulevya, Sheria yabMakosa ya Kimtandao na Sheria ya Utakasishaji wa Fedha Haramu.
Kwa upande wa Mkuu wa shule hiyo Mwalimu Mwaibingila amesema baada ya kupata elimu hiyo wamejipanga kuwa mabalozi wa kupinga matumizi ya madawa ya kulevya,ukatili wa kingono pamoja na makosa ya kimtandao kwa kuunda klabu mbalimbali.
"Natamani niwashawishi kituo Cha redio hapa Sumbawanga,Ili wanafunzi wa A level hasa waliopata mafunzo wakatoe elimu hii Kwa jamii nzima ya Rukwa kupitia redio chemchem"
Ameeleza kwamba shule hiyo kwa Sasa inaendelea uelimishaji jamii kuhusu mazingira na Mambo mbalimbali.
Mwisho








No comments: