Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania
(LRCT) imeibuka mshindi wa tatu kwa uandaaji na uwasilishaji bora wa hesabu za
mwaka kwa 2022 uliozingatia viwango vya taifa na kimataifa vya uhasibu katika
tuzo zilizotolewa na Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi (NBAA).
Tuzo hizo zimekabidhiwa na Waziri wa
nchi Ofisi ya Rais Ikulu Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe,CPA Jamal Kassim
Ali, usiku wa Desemba 1, 2023 katika ukumbi wa Hoteli ya APC Bunju Jijini Dar
es Salaam,wakati wa mkutano mkuu wa mwaka wa Wahasibu na Wakaguzi ambao
hushindanisha ubora katika uandaaji na uwasilishaji wa taarifa za hesabu za mwaka uliozingatia
viwango vya kitaifa na kimataifa vya Uhasibu.
Jumla ya Taasisi 98 ambazo
ziliwasilisha hesabu mwaka 2022 ziligawanywa katika makundi 18 ambapo Tume ya
Kurekebisha Sheria Tanzania walifanikiwa kuibuka mshindi wa tatu katika kundi
lake kipengele cha Taasisi za serikali kuu zilizoandaa kwa ubora hesabu za
mwaka 2022, huku nafasi ya pili ikishikwa na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana
na Dawa za kulevya (DCEA) na nafasi ya kwanza ikichukuliwa na Ofisi ya Msajili
wa Hazina (TRO).
Mkutano mkuu wa mwaka wa Bodi ya
Wahasibu na Wakaguzi (NBAA) hufanyika kila mwaka ambapo taarifa za hesabu kwa
Serikali, Taasisi na Mashirika huwasilishwa kwa bodi ya Taifa ya Uhasibu na
Ukaguzi kisha bodi huchagua kundi la
wataalam wabobezi na kukagua ubora wa uwasilishwaji kwa kuangalia kama viwango
vya kitaifa na kimataifa vimezingatiwa.













No comments: